• HABARI MPYA

    Sunday, April 13, 2014

    ITAFIKA WAKATI WACHEZAJI NYOTA WATAOGOPA KWENDA YANGA

    BARCELONA jana imehitimisha wiki ya machungu baada ya kufungwa bao 1-0 na Granada katika La Liga na kujiweka katika mazingira magumu ya kutetea ubingwa.
    Hali hiyo inatokea siku chache baada ya Barca kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki na wapinzani wao katika mbio za taji la La Liga, Atletico Madrid. 
    Bao la mapema la Yacine Brahimi ndilo lililowazamisha mabingwa wa zamani wa Ulaya na sifa zimuendee kipa Orestis Karnezis, aliyezuia michomo mingi akiichezea kwa mara ya pili klabu hiyo, akiwatoa kapa Lionel Messi na wenzake.  

    Barcelona inabaki na pointi zake 78 baada ya mechi 33 katika nafasi ya pili, nyuma ya vinara Atletico Madrid na wababe wao waliowatoa Ulaya, wenye pointi 79 za mechi 32, sawa na Real Madrid walio kileleni kwa wastani wa mabao.
    Barcelona ilifungwa ikiwa na wachezaji wake wote nyota, kikosi kilikuwa; Pinto, Montoya, Mascherano, Busquets aliyempisha Alexis dakika ya 74, Adriano aliyempisha Alba dakika ya 67, Song, Cesc Fabregas, Iniesta, Pedro, Messi na Neymar.
    Walipambana wanaume hao na kwa pamoja wote Neymar, Busquets na Messi wakaonyeshwa kadi za njano.
    Kwa Barcelona na Wakatalunya wote yamepita hayo, na wanashikana na timu yao kwa ajili ya mechi zijazo. Wanajua hiyo ndiyo soka. Hakuna cha kumshika mtu uchawi, sijui kahujumu wala nini, wanajua huo ndio mpira. Barca imetolewa na Atletico Ulaya na wiki hiyo hiyo inagongwa na Granada. Poa tu, ndiyo soka.
    Wakati nayatafakari matokeo hayo ya Barca wiki hii, nikakumbuka matokeo ya Yanga SC katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara wiki iliyopita.
    Yanga SC ilifungwa 2-1 na Mgambo JKT hivyo kuipisha kwa mbali kidogo Azam FC katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara.
    Siku hiyo safu ya ulinzi ya Yanga ilisababisha makosa ambayo wazi yaliigharimu timu- Kevin Yondan akimrudishia mpira kipa Juma Kaseja, ambaye alimpasia mchezaji wa Mgambo akafunga bao la kwanza.
    Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alifunga bao la kusawazisha kwa penalti, lakini Yondan tena akamchezea rafu mchezaji wa Mgambo na timu hiyo ya Jeshi ikapata bao la pili kwa penalti.
    Baada ya mechi hiyo, wachezaji kadhaa wa Yanga wamejikuta katika msukosuko wakituhumiwa kuhujumu timu na ingawa viongozi wa timu hiyo wanajifanya kutunza siri ya mgogoro na nyota wake hao, lakini zimevuja.
    Emmanuel Okwi analaumiwa hajitumi na inadaiwa wamekataa kumlipa baadhi ya fedha zake za usajili, naye ameamua kupumzika nyumbani.
    Sitaki kuzama sana kwenye hili la Okwi kama mchezaji binafsi, kwa kuwa si mada yangu leo, bali nataka kuwaambia viongozi wa Yanga- kama hawajui soka wajiuzulu, wawapishe watu wa mpira waongoze timu.
    Muuza mafuta, akauze mafuta, muuza magari akauze magari, muosha vyombo akaoshe vyombo- soka iongozwe na watu wa soka.
    Ni kuwadharau na kuwakebehi wana Yanga kuwaambia wamefungwa mabao 3-1 na watani wao Simba SC katika fete-mwaka mmoja tu tangu wafungwe 5-0.
    Hii maana yake pamoja na yote wanayofanya Yanga kuidhoofisha Simba ikiwemo kuchukua wachezaji wake nyota kila wakati wa usajili, lakini bado wameendelea kuwa vibonde kwa wapinzani wao hao.
    Sasa leo hata Yondan anaambiwa anahujumu Yanga, wakati iliwahi kuripotiwa alitoa taarifa za kutekwa na Ulimboka Mwakingwe akitaka amrejeshe Simba SC.
    Mbwembwe zote zile za usajili wa Okwi na maandamano kutoka Uwanja wa Ndege, leo kumbe ni mchezaji asiyejituma!
    Ally Mustafa ‘Barthez’ alionekana hafai baada ya kufungwa mara tatu katika sare ya 3-3 Simba SC wakitoka nyuma kwa 3-0, akasajiliwa Juma Kaseja, sasa naye vipi tena?    
    Lazima tukubali mpira una wenyewe- Yanga SC ina viongozi wenye fedha,  huwezi kukataa- lakini hakuna uhakika kama wanajua mpira au wanaelewa mipango ya mpira, wengi wao wanaonekana wapenda sifa tu kwenye kwenye vyombo vya habari, kujibebesha majina ya watu mashuhuri duniani sijui akina Sheikh Mansour. Lakini hawana lolote. 
    Uwekezaji mkubwa, uendeshaji wa timu kwa gharama kubwa, lakini michuano ya Afrika hawafiki popote- na kila siku siku kazi yao kuwapakazia ubaya wachezaji.
    Nani alisababisha Yanga SC ikafungwa 5-0 na Simba, Ni Nsajigwa Shadrack kweli? Hii watu wa Yanga wanajua na iko siku watu wataumbuka, kwenye mpira hakuna siri ya kudumu. 
    Leo asakamwe Okwi kwa Yanga kufungwa na Mgambo yeye akiwa uwanjani, lini Okwi alifunga Uwanja wa Mkwakwani tangu akiwa Simba SC?
    Simba wenyewe waliwahi kumlaumu kwa kushindwa kufunga dhidi ya Mgambo Mkwakwani mwaka juzi hadi akalazimika kujibizana nao.
    Tazama Barcelona, wiki hii imetolewa Ligi ya Mabingwa na kufungwa na Granada katika La Liga ikiwa na wachezaji wote wakubwa akiwemo Messi na Neymar, lakini maisha yanaendelea.  Yanga lazima wabadilike, vinginevyo itafika wakati wachezaji nyota wataogopa kwenda katika timu yao kwa tuhuma za ovyo ovyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ITAFIKA WAKATI WACHEZAJI NYOTA WATAOGOPA KWENDA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top