• HABARI MPYA

    Saturday, April 19, 2014

    SIMBA NA YANGA LEO UTAMU PALE PALE...NANI ATAKABA MESSI, NANI ATAMZUIA NGASSA...TAMBWE, KAVUMBANGU JE?

    NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo zitawaka moto kwa mpambano wa watani wa jadi, Simba na Yanga SC wa kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2013/2014.
    Pambano hilo linakuja wakati tayari nafasi tatu za juu zimekwishapangika, yaani kuanzia ubingwa, Azam FC, mshindi wa pili, Yanga SC na wa tatu Mbeya City, lakini Simba SC iliyo katika nafasi ya nne, itashuka iwapo itafungwa Jumamosi ya leo na Kagera Sugar ikaifunga Coastal Union mjini Tanga.
    Hii inamaanisha mchezo wa leo ni muhimu zaidi kwa Simba SC kulinda heshima, baada ya kukosa nafasi mbili za juu, ambazo zingewapa tiketi ya kucheza michuano ya Afrika mwakani, basi angalau wapiganie nafasi ya nne baada ya kuzidiwa kete na Mbeya City katika nafasi ya tatu.
    Lakini Yanga SC umuhimu wa mchezo huu kwao uko wapi, ikiwa tayari wana tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho  hawawezi kupata zaidi wala kupungukiwa katika ambayo wamekwishavuna hadi sasa katika Ligi Kuu.
    Wababe tena? Simba SC iliifunga Yanga 3-1 mara ya mwisho zilipokutana, je leo wataendeleza ubabe?

    Kikubwa ni heshima, ni visasi ambavyo ndio deni kubwa kwa Yanga SC mbele ya mahasimu wao- kipigo cha 6-0 mwaka 1977, 5-0 za 2012 na 3-1 za Desemba mwaka jana, bado vinawaumiza wapenzi wa timu hiyo.

    Fikra za viongozi wa sasa wa Yanga SC chini ya Mwenyekiti,Yussuf Mehboob Manji ni kulipa kipigo cha 5-0 cha Mei 6, mwaka 2012 maana yake bado wapo kwenye mawindo hayo na ndiyo maana waliweka kambi katika hoteli maridadi eneo la Mbezi, Dar es Salaam.

    Lakini kauli ya Mwenyekiti wa Yanga SC, Manji baada ya timu hiyo kufungwa 3-1 Desemba 21, mwaka jana kwamba mechi ambazo hazina umuhimu kimatokeo haziwaumizi kichwa hata wakifungwa, inaleta wasiwasi kama timu hiyo itaweza kufurukuta mbele ya mahasimu wao.


    Toa wawili: Emmanuel Okwi wa kwanza kulia waliosimama na Haruna Niyonzima wa kwanza kushoto waliochuchumaa hawapo kambini

    MECHI ZA WATANI TANGU MWAKA 2010:

    APRILI 18, 2010
    Simba Vs Yanga
    4-3
    WAFUNGAJI:
    SIMBA: Uhuru Suleiman dk 3, Mussa Mgosi dk 53 na 74, Hillary Echesa dk 90+  
    YANGA: Athumani Iddi dk 30, Jerry Tegete dk 69 na 89 
    OKTOBA 16, 2010:
    Yanga Vs Simba
    1-0
    MFUNGAJI: Jerry Tegete dk 70
    MACHI 5, 2011
    Simba Vs Yanga
    1-1
    WAFUNGAJI:
    YANGA: Stefano Mwasyika (penalti) dk 59. 
    SIMBA:  Mussa Mgosi dk 73.
    (Refa Orden Mbaga alizua tafrani uwanjani, kwanza kwa kulikataa bao la kusawazisha la Simba, kisha akalikubali baada ya kujadiliana na msaidia wake namba moja)
    OKTOBA 29, 2011
    Yanga 1-0 Simba
    MFUNGAJI: Davies Mwape dakika ya 75
    MEI 6, 2012
    Simba 5-0 Yanga SC
    WAFUNGAJI: 
    Emmanuel Okwi (dk 2 na 62), Felix Sunzu (penalti 56), Juma Kaseja (penalti dk 67) na Patrick Mafisango (penalti dk 72)
    (Ligi Kuu)
    OKTOBA 3, 2013
    Simba 1-1 Yanga SC
    WAFUNGAJI:
    Simba SC: Amri Kiemba dk3
    Yanga SC: Said Bahanuzi dk65
    (Ligi Kuu)
    MEI 18, 2013
    Yanga 2-0 Simba SC
    WAFUNGAJI: Didier Kavumbangu dk 5 na Hamisi Kiiza dk 62.
    OKTOBA 20, 2013
    Yanga SC 3-3 Simba SC
    WAFUNGAJI:
    Yanga SC: Mrisho Ngassa dk15, Hamisi Kiiza dk36 na 45
    Simba SC: Betram Mombeki dk54, Joseph Owino dk58 na Gilbert Kaze dk85.
    (Matokeo haya ni ya mechi za Ligi Kuu pekee)
    “Tuliamua kucheza kumfurahisha  mdhamini TBL, tumefungwa lakini bado tunaongoza ligi, hatujapoteza pointi hata moja, ile ilikuwa fete tu,”alisema Manji akizungumza na Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
    Yanga SC inapewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo wa leo, kwa sababu inaonekana bora kuliko mahasimu wao, Simba SC ambao hawakuwa katika msimu mzuri kwa mara nyingine, wakiporomoka zaidi kuliko msimu uliopita.
    Tangu mwaka 2001 Simba haijamaliza Ligi Kuu nje ya nafasi mbili za juu, lakini kwa mara ya kwanza msimu huu wamemaliza katika nafasi ya tatu na kama watapoteza mechi ya leo watashuka hadi ya nne.
    Lakini ukirejea mchezo uliopita wa watani, ambao ulikuwa wa Nani Mtani Jembe unaweza kujionea Simba SC ina timu ya kuifunga Yanga tena na kuifunika hadi uwanjani pia. Nani katika mabeki wa Yanga anaweza kumzuia kabisa Ramadhani Singano ‘Messi’ asifanye yake?
    Vipi kuhusu Amisi Tambwe, mfungaji bora wa Ligi Kuu- au winga mwingine machachari, Haroun Chanongo.
    Nenda katika safu ya kiungo, kocha Zdravko Logarusic ana wakali kama Said Ndemla, Amri Kiemba, Jonas Mkude na Awadh Juma wakati safu ya ulinzi inayoongozwa na Mkenya Donald Mosoti na Mganda Joseph Owino nayo ni madhubuti pia.
    Kipa mkongwe Ivo Mapunda anapoamua kufanya kazi langoni hata Yanga wanajua kumfunga ni kazi- wasiwasi upo kwa mabeki wa pembeni wa Wekundu hao wa Msimbazi, kidogo Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ akiwa fiti anaweza kukabiliana na kasi ya winga machachari wa wana Jangwani, Simon Msuva.
    Nahodha Nassor Masoud ‘Chollo’ msimu huu amekuwa akijiuguza zaidi nje ya Uwanja, ingawa sasa amepona, lakini haijulikani kama yupo katika ubora wa kuanza. William Lucian ‘Gallas’ ndiye beki mwingine wa kulia aliyekuwa kambini Zanzibar.
    Yanga SC mabeki wa pembeni wote wanaotumika kwa sasa ni wazuri, ila leo watatakiwa kuwa wazuri zaidi wakipambana na Chanongo na Messi. Hakuna shaka kuhusu kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ huyo ni bora na hodari langoni.
    Kevin Yondan amerudishwa kikosini na alicheza dhidi ya JKT Oljoro, Mbuyu Twite na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ pia wapo- je, kocha Hans van der Pluijm ataipangaje timu yake leo. Juma Abdul ataanzia benchi, kulia acheze Twite ili katikati wacheze Yondan na Cannavaro? Tutajua jioni.       
    Frank Domayo atacheza kiungo cha chini na juu yake atacheza Hassan Dilunga, wakati washambuliaji bila shaka wataanza Hamisi Kiiza na Didier Kavumbangu na pembeni watakimbiza Mrisho Ngassa na Msuva.
    Ngassa amerudi katika kiwango chake na anacheza kwa kasi sana hivi sasa, maana yake Yanga nayo itakuwa hatari pembeni leo.
    Kwa Yanga SC, bila shaka Hussein Javu atatokea benchi kuingia kuongeza nguvu, huyo ni mtu hatari sana, wakati kwa Simba SC Zahor Pazi anaweza kuingizwa baadaye, naye anatisha na akipata nafasi hiyo atataka kuwaonyesha kitu mashabiki wa Simba SC.
    Ladha ya mchezo wa watani inabaki pale pale, pamoja na kuonekana kwamba umepoteza mvuto kwa sababu nafasi tatu za juu zimekwishapata wenyewe.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA YANGA LEO UTAMU PALE PALE...NANI ATAKABA MESSI, NANI ATAMZUIA NGASSA...TAMBWE, KAVUMBANGU JE? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top