• HABARI MPYA

    Friday, August 01, 2014

    STARS WAPATA MSUKOSUKO ANGANI, NDEGE YA AFRIKA KUSINI YAKORIFISHA IKIELEKEA MAPUTO, YAGEUZA NA KUREJEA JOHANNESBURG

    Na Mahmoud Zubeiry, MAPUTO
    KIKOSI cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilipata msukosuko angani kwenye ndege kikitokea Afrika Kusini baada ya ndege ya shirika la nchi hiyo kugeuza kurudi Johannersburg baada ya rubani kubaini hitilafu.
    Stars iliarajiwa kufika Maputo, Msumbiji Saa 8:40 mchana kwa saa za hapa, lakini wakiwa nusu ya safari walitangaziwa kutokea matatizo ambayo yaliifanya irejee Uwanja wa Ndege wa O R Tambo kwa matengenezo.
    Baada ya matengenezo ya takriban saa moja, ndege hiyo ilipaa tena na kufika Maputo Saa 11:30 za huku, tayari kwa mchezo wa marudiano hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Morocco. 
    Kocha wa Stars, Mart Nooij kushoto akizungumza na Waandishi wa Habari
    Beki wa Stars, Aggrey Morris akiwasili Maputo
    Kutoka kulia Haroun Chanongo, Simon Msuva na Mrisho Ngassa
    Mwinyi Kazimoto kwenye basi kuelekea hotelini Maputo 

    Katika mchezo huo utakaofanyika Jumapili, Stars inahitaji ushindi wa ugenini au sare ya kuanzia mabao 3-3 ili kusonga mbele, baada ya awali kulazimishwa sare ya 2-2 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema begi la jezi ambazo zitatumika kwenye mchezo wa Jumapili limesahaulika Johannesburg na tayari wametoa taarifa kwa wahusika, Shirika la ndege la Afrika Kusini ili liletwe kesho.
    Wachezaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu watawasili kesho asubuhi wakitokea Afrika Kusini.
    Baada ya kuwasili, kocha Mkuu wa Stars, Mart Nooij raia wa Uholanzi aliwaambia Waandishi wa Habari kwamba wachezaji wake wote wako fiti kuelekea mchezo wa Jumapili na wenyeji Mambas.
    Amesema hana majeruhi hata mmoja kikosini mwake na kambi yao ya siku mbili nchini Afrika Kusini ilikuwa nzuri na amewataka Watanzania wawe na imani na timu yao kuelekea mchezo huo.
    Hata hivyo, Nooij alisema wachezaji wake walipata hofu baada ya hitilafu zilizotokea kwenye ndege, lakini imechangia pia kuwajenga kisaikolojia.
    Nooij alipokewa vizuri na raia wa Msumbiji kuanzia wafanyakazi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Maputo kutokana na kukumbuka kazi yake nzuri alipokuwa kocha wa Mambas kabla ya kwenda Ethiopia na baadaye Tanzania.
    Kiungo mwandamizi wa timu hiyo, Amri Kiemba amesema wamekuja Msumbiji kwa ajili ya kitu kimoja tu, kuhakikisha wanashinda na kusonga mbele.
    Beki Aggrey Morris ambaye anaweza kuanza Jumapili badala ya Kevin Yondan, amesema; “Kambi ya Afrika Kusini ilikuwa nzuri, tulifanya mazoezi mazuri na wachezaji wako fiti na wana ari ya ushindi,”.
    Kwa ujumla wachezaji wa Stars wamewasili wakiwa vizuri jioni ya leo pamoja na misukosuko waliyoipata njiani. 
    Katika mchezo wa kwanza, Dar es Salaam mabao ya Stars yalifungwa na kiungo wa Azam FC, Khamis Mcha ‘Vialli’ aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mrisho Ngassa. 
    Dakika 45 za kwanza zilimalizika bila bao na kipindi cha pili, Msumbiji walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 47 kwa penalti iliyokwamishwa nyavuni na Elias Pelembe baada ya Kevin Yondan kumcheza rafu kwenye eneo la hatari. Mcha aliisawazishia Stars bao hilo dakika ya 65 akimalizia krosi nzuri ya Thomas Ulimwengu.
    Mcha tena akaifungia Stars bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 71 kwa penalti, baada ya mabeki wa Mambas kumchezea rafu Mbwana Samatta kwenye eneo la hatari.
    Stars iliongeza mashambulizi langoni mwa Msumbiji na kukosa mabao kadhaa ya wazi. Msumbiji walizinduka na kufanya shambulizi zuri lililowapatia bao la kusawazisha dakika ya 87 kupitia kwa Isaac Carvalho aliyetokea benchi pia.
    Stars sasa itajitaji ushindi wa ugenini ili kusonga mbele, au sare ya kuanzia mabao 3-3, wakati wenyeji wanaweza kunufaika na sare ya 1-1 au 0-0. Ikiwa 2-2 tena, mshindi ataamuliwa kwa mikwaju ya penalti.
    Stars iliyofika hatua hii baada ya kuitoa Zimbabwe kwa jumla ya mabao 3-2 ikishinda 1-0 nyumbani na sare ya 2-2 Harare, ikifanikiwa kuitoa Msumbiji itapangwa katika Kundi C ambalo lina timu za Zambia, Cerpe Verde na Niger zilizofuzu moja kwa moja hatua hiyo, kuwania tiketi ya Morocco mwakani. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS WAPATA MSUKOSUKO ANGANI, NDEGE YA AFRIKA KUSINI YAKORIFISHA IKIELEKEA MAPUTO, YAGEUZA NA KUREJEA JOHANNESBURG Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top