• HABARI MPYA

    Monday, September 15, 2014

    AYA 15 ZA SAID MDOE: CHAZ BABA NA TWANGA PEPETA NI KAMA MATE NA ULIMI?

    MSANII kusalimia kisanii kwenye jukwaa la bendi nyingine ni jambo la kawaida, lakini Chaz Baba anaweza kuwa anaandika rekodi ya aina yake bila ya yeye mwenyewe kujijua.
    Mwimbaji huyu wa Mashujaa Band, amekuwa na kawaida ya kusalimia kisanii kwenye majukwaa ya bendi kadhaa, hana hiyana wala choyo kwenye hili, lakini unapozungumzia yeye kupanda jukwaa la Twanga, hakuna ubishi kuwa anakuwa anatekenya hisia za watu wengi.
    Alhamisi iliyopita, Chaz alikuwepo Maisha Club kushuhudia Twanga Pepeta wakifanya vitu vyao.

    Hakuvumilia, akapanda jukwaani na kushiriki kuimba wimbo mpya kabisa “X-Michepuko” uliotungwa na Msafiri.
    Ni wimbo ambao Chaz Baba haujui kabisa, lakini bado akaweza kudumbukiza hisia zake ndani ya ngoma hiyo na kusisimua mashabiki wa bendi hiyo.
    Inakumbukwa Chaz Baba aliwahi kung’ara kwa sana tu na Twanga Pepeta kabla ya kuhamia Mashujaa Band na kufanya bendi hizo ziwe na upinzani wa aina yake.
    Kila Chaz Baba anapopanda jukwaa la Twanga Pepeta, mashabiki wa bendi hiyo hufurahi na kujifariji kwa msemo wa “Nyumbani ni Nyumbani” wakimaanisha kuwa siku siku zote mtoto akienda kujitegemea, basi lazima arejee nyumbani kusalimia wazazi au walezi wake.
    Lakini mashabiki wa Twanga huwa wanakwenda mbali zaidi kwa kuamini kuwa siku moja mwimbaji huyo aterejea kuitumikia Twanga Pepeta.
    Kwanini hapo juu nimesema Chaz Baba anaweza kuwa anajitengenezea historia bila yeye mwenyewe kujijua? Ni kwasababu kwa sasa yeye ndio anakuwa mwimbaji aliyeihama Twanga anayeongoza kwa kulisalimia kisanii jukwaa la bendi hiyo kuliko mwimbaji mwingine yeyote yule.
    Tangu Chaz Baba aondoke Twanga kiasi cha miaka mitatu iliyopita, ameshapanda jukwaa la bendi hiyo kwa zaidi ya mara 10.
    Lakini pia aliwahi kufanya kitu ambacho hadi leo ni gumzo, pale alipotoka kwenye sherehe za harusi yake kwenye ukumbi wa Mirando Sinza jijini Dar es Salaam na kwenda kupanda jukwaa la Twanga Pepeta Mango Garden akiwa na mkewe tena wakiwa bado wako na nguo zao za harusi.
    Wakati MC wa sherehe ya harusi yao iliyofanyika mwezi August mwaka jana, Chiki Mchoma akitangaza kuwa sasa maharusi wanakwenda kupumzika, kila mtu aliamini hivyo, lakini mtu na mkewe hao kiguu na njia hadi Mango Garden kutumbuiza kwenye jukwaa la Twanga Pepeta.
    Nimekuwa nikijiuliza sana: Hivi Chaz Baba bila kupanda jukwaa la Twanga haiwezekani? Hajui kuwa kwa kufanya hivyo anainufaisha bendi pinzani? Hajui kuwa anawapa la kusema mashabiki wa Twanga? Hajui kuwa wasiotakia mema Mashujaa pamoja na yeye mwenyewe wanatamba kuwa kafuata pesa za kutunzwa jukwaani (ambazo eti kule Mashujaa hazipati)? Huwa sipati majibu kwa kweli.
    Nina uhakika wa asilimia mia moja kuwa baadhi ya viongozi wa Mashujaa Band hawavutiwi na hali hiyo. Nina Uhakika baadhi ya wanamuziki wa Twanga Pepeta hawavutiwi na hali hiyo. 
    Nina uhakika Chaz anajua kuwa si kila mtu mtu ndani ya Mashujaa na Twanga anafurahi kwa yeye kupanda jukwaa la Twanga Pepeta, lakini bado hilo halimtishi na ndio maana mwisho wa siku najiuliza tena: Chaz Baba na Twanga ni kama mate na ulimi? 
    Je ni sahihi anachofanya Chaz Baba? Si mimi wala wewe tunayeweza kujua hilo, ni yeye na mwajiri wake ndio wanajua kama ni sahihi au la. Tukutane Jumatatu ijayo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AYA 15 ZA SAID MDOE: CHAZ BABA NA TWANGA PEPETA NI KAMA MATE NA ULIMI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top