• HABARI MPYA

    Monday, September 15, 2014

    LOGARUSIC AIPELEKA PUTA SIMBA SC, TFF YAWAPA SIKU 14 KUMALIZANA NAYE, VINGINEVYO…

    Na Boniface Wambura, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikishola Soka Tanzania (TFF), imewapa siku 14 Simba SC kumaliza mgogoro wao na kocha wao wa zamani, Mcroatia Zdravko Logarusic.
    Taarifa ya TFF leo, imesema kwamba iwapo pande hizo mbili zitashindwa kufikia mwafaka ndani ya siku 14, suala hilo litarejea tena mbele ya Kamati.
    Logarusic aliyewakilishwa na mwanasheria wake Dickson Sanga anailalamikia klabu hiyo kwa kuvunja mkataba kinyume cha taratibu, hivyo kutaka Simba imlipe dola 6,000 kwa kuvunja mkataba, na pia kulipa dola 50,000 ikiwa ni fidia maalumu ya madhara yaliyotokana na uvunjwaji huo.
    Logarusic kulia wakati anasaini Mkataba mpya na Simba SC Juni mwaka huu, kabla ya kufukuzwa mwezi mmoja na ushei baadaye 

    Simba SC ilimfukuza Logarusic mwezi uliopita baada ya kufanya kazi tangu Desemba mwaka jana, ikidai kwamba haendani na maadili ya klabu hiyo.
    Aidha, Kamati pia imepitisha usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza huku wenye kasoro ndogondogo klabu zao zikitakiwa kuziondoa ili waweze kupatia leseni za kucheza ligi msimu huu wa 2014/2015.
    Kasoro hizo ni kufikia makubaliano na klabu ambazo wachezaji husika wametoka, kuwafanyia uhamisho (transfer) na kulipa ada za uhamisho. Kamati vilevile ilibaini wachezaji wengi hawakufanyiwa uhamisho kama kanuni za ligi hizo zinavyoelekeza.
    Hivyo, klabu ambazo hazitakuwa zimeondoa kasoro hizo kwa wachezaji wao leseni zao zitazuiliwa mpaka watakapokuwa wamekamilisha kila kitu. Ni wachezaji wenye leseni tu ndiyo watakaoruhusiwa kucheza mechi za ligi.
    Klabu za African Lyon, African Sports, Ashanti United, Coastal Union, Kiluvya United, Majimaji, Mji Mkuu, Polisi Dodoma, Polisi Morogoro, Red Coast na Stand United ziliwawekea pingamizi wachezaji mbalimbali kwa kutofanyiwa uhamisho.
    Kuhusu Ike Bright Obina wa Nigeria aliyewekewa pingamizi na African Lyon dhidi ya Coastal Union, Kamati imezitaka klabu hizo kufikia makubaliano, na zikishindwa mchezaji huyo atabaki African Lyon.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LOGARUSIC AIPELEKA PUTA SIMBA SC, TFF YAWAPA SIKU 14 KUMALIZANA NAYE, VINGINEVYO… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top