• HABARI MPYA

    Sunday, September 28, 2014

    YANGA SC YAILAZA 2-1 PRISONS, COUTINHO APIGA BONGE LA BAO, MSUVA AFUNGA LA USHINDI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imepata ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuilaza Prisons ya Mbeya mabao 2-1 jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mbrazil Andrey Coutinho alikuwa wa kwanza kuipatia Yanga SC bao dakika ya 34 kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa zaidi ya mita 25, baada ya Mrisho Ngassa kuangushwa.
    Yanga SC ingeweza kwenda kupumzika na mabao zaidi, kama mshambuliaji wake tegemeo kwa sasa, Mbrazil, Genilson Santana Santos ‘Jaja’ angetumia vizuri nafasi mbili nzuri alizotengenezwa.
    Andrey Coutinho akishangilia baada ya kuifungia Yanga SC bao la kwanza

    Kwanza ilikuwa ni krosi ya karibu ya Ngassa dakika ya 31 kutoka upande wa kulia, lakini Jaja akachelewa na kipa Mohamed Omar akapangua mpira juu ya kichwa cha Mbrazil huyo.
    Baadaye, dakika ya 42 Niyonzima alimtoka vizuri beki wa Prisons na kutia krosi nzuri ya juu, ambayo Jaja pamoja na kuiunganisha kwa kichwa kuelekea nyavuni, lakini ikaokolewa karibu na mstari wa lango.
    Kwa ujumla, Yanga SC inayofundishwa na Mbrazil Marcio Maximo, ilicheza vizuri kipindi cha kwanza, wakati Prisons pamoja na kuonyesha upinzani, lakini ilioneiana kuzidiwa.  
    Prisons ilimaliza kipindi cha kwanz aikiwa pungufu, baada ya beki wake, Jacob Mwakalobo kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 39 baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na refa Andrew Shamba wa Pwani, kufuatia kumchezea vibaya Ngassa.
    Mshambuliaji wa Yanga SC, Mrisho Ngassa akipambana na beki wa Prisons, Jacob Mwakalobo leo Uwanja wa Taifa

    Kipindi cha pili, Prisons walibadlika na kuanza kusukuma mashambulizi yenye uhai langoni mwa Yanga SC- hali ambayo iliwafanya wapate bao la kusawazisha dakika ya 67, mfungaji Ibrahim Kahaka aliyetokea benchi ambaye alimalizia pasi ya Jeremiah Juma.
    Lakini bao hilo halikudumu, kwani dakika mbili baadaye, Simon Msuva aliifungia Yanga SC bao la ushindi akimalizia krosi maridadi ya Ngassa kutoka upande wa kulia.
    Baada ya hapo, timu hizo zilianza kushambuliana kwa zamu na Prisons walilalamika kunyimwa penalty baada ya beki na Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuunawa mpira kwenye boksi.
    Jaja akimpongeza Msuva baada ya kufunga bao la ushindi

    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Edrwad Charles, Kevin Yondan/Rajab Zahir dk77, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga/Hamisi Thabit dk54, Genilson Santana ‘Jaja’, Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho/Simon Msuva dk58.   
    Prisons; Mohamed Omar, Salum Lameya, Laurian Mpalile/Boniface Hau dk74, Nurdin Chona, Lugano Mwangama, Jumanne Elfadhil, Meshack Olest/Julius kwangwa dk35, Freddy Dungu, Jacob Mwakalobo, Amin Omary/Ibrahim Kahaka dk53 na Jeremiah Juma.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAILAZA 2-1 PRISONS, COUTINHO APIGA BONGE LA BAO, MSUVA AFUNGA LA USHINDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top