• HABARI MPYA

    Thursday, October 16, 2014

    SIMBA SC YAREJEA DAR ‘CASSILAS’ AMEBEBWA KWENYE KITI CHA WALEMAVU

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imerejea Alfajiri ya leo kutoka Afrika Kusini ilipokuwa imeweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu wao, Yanga SC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    Kipa Hussein Sharrif ‘Cassilas’ amerejea anasukumwa kwenye kiti cha walemavu kutokana na kuumia mguu katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Orlando Pirates Jumamosi iliyopita.
    Lakini msafara mzima unaonekana kuwa vizuri kuelekea kwenye mchezo huo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara keshokutwa.
    Hata hivyo, msafara uliowasili hauhusishi wachezaji walioondoka Jumatatu akiwemo kipa Ivo Mapunda, ambao watawasili baadaye mchana leo.
    Kipa Hussein Sharrif 'Cassilas' akisukumwa kwenye kiti cha walemavu baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam Alfajiri ya leo

    Simba SC imerejea baada ya jana kukamilisha mechi zake za kirafiki za kujipima nguvu katika kambi yake ya Afrika kwa kufungwa mabao 2-0 na Jomo Cosmos mjini Johannesburg jioni.
    Pamoja na kufungwa na timu hiyo ya Daraja la Kwanza, inayomilikiwa na kufundishwa na gwiji wa soka Afrika Kusini, Jomo ‘Black Prince’ Sono, Simba SC ilicheza soka ya kuvutia.
    Huo ulikuwa mchezo wa tatu kwa Simba SC katika kambi yake hiyo tangu iwasili Oktoba 8, mwaka huu, mchezo wake wa kwanza, Simba SC ililazimishwa sare ya bila kufungana na Orlando Pirates kabla ya kufungwa mabao 4-2 na Bidvest Wits, au Wits University.
    Simba SC ilitarajiwa kuingia kambini katika hoteli Upplands eneo la Changanyikeni, Dar es Salaam- ingawa haijulikani mazoezi watafanya wapi, kwa sababu Uwanja waliokuwa wakiutumia kabla ya kwenda Afrika Kusini wa Boko Veterani, sasa unatumiwa na Yanga SC.
    Yanga SC imeweka kambi hoteli ya Landmark, Kunduchi, Dar es Salaam tangu Jumatatu.  
    Kocha Patrick Phiri akiwa mbele kwenye gari tayari kwa safari ya kambini baada ya kuwasili Dar es Salaam
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAREJEA DAR ‘CASSILAS’ AMEBEBWA KWENYE KITI CHA WALEMAVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top