• HABARI MPYA

    Saturday, November 01, 2014

    KIVUMBI LIGI KUU LEO, SIMBA NA YANGA MIKONONI MWA WAKATA MIWA, AZAM NA VIBONDE NDANDA MTWARA

    MECHI ZA LIGI KUU BARA WIKIENDI HII 

    Novemba 1, 2014:
    Kagera Sugar Vs Yanga SC
    Coastal Union Vs Ruvu Shooting
    JKT Ruvu Vs Polisi Moro
    Ndanda FC Vs Azam FC
    Stand United Vs Prisons
    Mtibwa Sugar Vs Simba SC
    Novemba 2, 2014
    Mgambo JKT Vs Mbeya City

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaendelea leo kweye viwanja sita, macho na masikio ya wengi zadi yakielekezwa Morogoro na Bukoba, ambako vigogo Simba na Yanga watakuwa wageni wa timu za kampuni za Sukari.
    Yanga SC watakuwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba kumenyana na wenyeji Kagera Sugar, wakati Simba SC watakuwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kucheza na wenyeji, Mtibwa Sugar.
    Yanga SC wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa tayari wamevuna pointi 10 katika mechi tano na kuwa moja ya timu tatu zinazofukuzana kileleni mwa ligi hiyo, pamoja na Azam FC na Mtibwa Sugar.
    Mabingwa watetezi, Azam FC wapo Mtwara leo dhidi ya Ndanda

    Simba SC wana kazi, kwa sababu Mtibwa Sugar ndiyo inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 13 ikiwa imeshinda mechi zake nne kati ya tano na moja kutoa sare.
    Simba SC inakutana na Mtibwa ikiwa katika wakati mgumu na kocha wake Mkuu, Mzambia Patrick Phiri tayari amekwishaambiwa kama hatashinda mechi mbili kuanzia leo, basi anaweza kuondolewa kazini.
    Tayari wachezaji watatu wa nafasi za kiungo, Amri Kiemba, Haroun Chanongo na Shaaban Kisiga ‘Malone’, wameondolewa kambini kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.  Na Simba SC haijashinda mechi hata moja ya Ligi Kuu msimu huu, ikitoa sare zote tano.
    Mchezo mwingine unaotarajiwa kuteka hisia za watu ni kati ya Ndanda FC watakaoikaribisha Azam FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara. Ndanda wamepitia wimbi la matokeo mabaya kiasi cha kubadilisha benchi lake la ufundi wiki iliyopita na leo watakuwa wanapigania ushindi wa kwanza baada ya kupoteza mechi nne mfululizo, mbili nyumbani. 
    Azam FC yenye pointi 10 ambao ndio mabingwa watetezi, watakuwa wanajaribu kuzinduka baada ya Jumamosi kuchapwa bao 1-0 na JKT Ruvu, hicho kikiwa kipigo cha kwanza baada ya mechi 38 ndani ya misimu miwili.
    Mechi nyingine, Coastal Union watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, JKT Ruvu wataikaribisha Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na Stand United watakuwa wenyeji wa Prirons Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
    Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mchezo mmoja tu, Mbeya City ‘iliyobaki jina’ itakuwa mgeni wa Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIVUMBI LIGI KUU LEO, SIMBA NA YANGA MIKONONI MWA WAKATA MIWA, AZAM NA VIBONDE NDANDA MTWARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top