• HABARI MPYA

    Monday, December 15, 2014

    SIMBA SC YAMALIZA KAZI, KITASA CHA MAANA KESSY CHASAINI MIEZI 18 MSIMBAZI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imefunga usajili wake wa dirisha dogo kwa kumsaini beki wa kulia wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Hassan Ramadhani Kessy.
    Kessy amesaini usiku huu Mkataba wa miezi 18 baada ya mvutano wa muda mrefu na klabu hiyo juu ya dau.
    Zaidi ya mara tatu, Kessy alikwishakutana mezani na uongozi wa Simba SC bila kufikia maafikiano na baada ya mvutano huo uliodumu kwa takriban mwezi mzima, leo mambo yameisha.
    “Napenda kuwataaarifu wapenzi na wanachama wa Simba SC kwamba tumemsajili beki Kessy, ambaye ni pendekezo la mwalimu wetu (Patrick Phiri),”amesema Makamu wa Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’.
    Kessi (katikati) akisani Mkataba wa Simba SC leo. Kulia anayeshuhudia ni Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Kaburu na kushoto ni mwakilishi wa mchezaji, Athumani Tippo
    Kaburu amesema kwamba baada ya kumpata Kessi wanadhani sasa kikosi chao kimekamilika na wanaelekeza nguvu zao katika maandalizi kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Kessy anakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na Simba SC katika dirisha dogo, baada ya Waganda beki Juuko Murushid na washambuliaji Dan Sserunkuma na Simon Sserunkuma.
    Murushid amesaini miaka mitatu, wakati akina Sserunkuma wamesaini miaka miwili kila moja.
    Simba SC imewatema Warundi kiungo Pierre Kwizera na mshambuliaji Amisi Tambwe aliyehamia kwa mahasimu, Yanga SC baada ya kuwasajili Waganda hao.
    Simba SC ililazimika kuwatema Warundi hao ili kukidhi matakwa ya kanuni ya Usajili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ya wachezaji watano wa kigeni.
    Murushid na akina Sserunkuma wanaungana na Waganda wenzao, beki Joseph Owino na mshambuliaji Emmanuel Okwi kukamilisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAMALIZA KAZI, KITASA CHA MAANA KESSY CHASAINI MIEZI 18 MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top