• HABARI MPYA

    Wednesday, December 17, 2014

    TUNA NINI SISI, MAJANGA MATUPU NA CECAFA YETU!

    TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Zambia jana imeifunga Zimbabwe mabao 3-0 mjini Bulawayo na kutwaa Kombe la COSAFA (Shirikisho la Soka Kusini mwa Afrika).
    Young Chipolopolo ilianza na moto wake mwanzo mwisho kwenye mashindano hayo, ikifunga jumla ya mabao 19 baada ya kuichapa Afrika Kusini 6-1, Namibia 2-0, Lesotho 4-0 na Malawi 4-0 katika Nusu Fainali.
    Mabao yote matatu jana waliyapata kipindi cha pili kupitia kwa Patrick Ngoma, Harrison Chisala na Solomon Sakala.
    Zimbabwe pia wanapaswa kumshukuru kipa wao, Kelvin Shangiwa aliyeokoa michomo ya hatari ya kiungo Patson Daka mara mbili dakika ya 14 na 30.

    Ngoma aliifungia Zambia bao la kwanza dakika ya 53 akimalizia krosi ya Crispin Sakulanda, kabla ya Chisala kufunga la pili dakika nne baadaye akiunganisha krosi ya Charles Shezongo na Solomon Daka kuhitimisha ushindi huo dakika ya 77 kwa penalti bsaada ya Sakulanda kuangushwa na Leslie Lunga aliyetolewa kwa kadi nyekundu.
    Young Chipolopolo sasa itatetea taji hilo mwakani nyumbani wakati Zambia watakapokuwa wenyeji Desemba 2015.
    Wakati huo huo, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) mwishoni mwa wiki lilikuwa na Mkutano wa kujadili matatizo yao.
    Katika Mkutano huo, CECAFA wameamua rasmi kuachana na ndoto za kufanya Kombe la Challenge mwaka huu, na badala yake kuelekeza nguvu katika mashindano ya mwakani.
    Taarifa ya Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye  kwa BIN ZUBEIRY, imesema kwamba hayo yamefikiwa katika Mkutano Mkuu wa dharula wa bodi hiyo uliofanyika Jumapili mjini Nairobi, Kenya chini ya Mwenyekiti wake, Mhandisi Leodegar Chillah Tenga.
    Mkutano huo, ulihudhuriwa na viongozi wakuu 11 kati ya 12 wa Vyama na Mashirikisho ya Soka Afrika Mashariki na Kati, Jamal Malinzi (Tanzania), Sam Nyamweya (Kenya), Moses Magogo (Uganda), Vincent Nzamwita (Rwanda), Goc Chabur (Sudan Kusini), Reverien Ndikuriyo (Burundi), Abdiqaani Saed (Somalia), Tesfaye Gebreyesus (Eritrea), Juneidi Basha (Ethiopia) Ahmed Eltrifi (Sudan) na Ravia Idarius (Zanzibar).
    Baada ya saa nne za michango na mijadala, CECAFA imefikia uamuzi wa kubadilisha muundo wa mashindano yake ili kupunguza gharama na kuongeza mvuto wake. 
    Pamoja na hayo, CECAFA wamekubaliana kuendelea kumuunga mkono, Rais wa sasa CAF, Issa Hayatou na rais wa FIFA, Sepp Blatter katika uchaguzi wa mwakani. 
    Michuano ya Challenge ilipangwa kufanyika Ethiopia mwaka huu, lakini wenyeji hao wakajitoa dakika za mwishoni na jitihada za CECAFA kupata nchi mbadala wa kuandaa mashindano hayo hazikufanikiwa.
    Tayari Rwanda imepewa uenyeji wa Challenge ya mwakani, kama sehemu ya kujipima kabla ya kuipokea michuano ya CHAN. 
    CECAFA kwa sasa inamudu kuendesha mashindano mawili tu, Kombe la Kagame na Chgallenge ambayo mwaka huu haikufanyika.
    Wote tunaamini soka ya vijana ndiyo chimbuko la nyota wa baadaye. Ndiyo mustakabali mzima wa timu bora ya taifa ya baadaye, lakini huku CECAFA tulikwishaacha siku nyingi upuuzi wa soka ya watoto.
    Wenzetu COSAFA wanapiga hatua na mashindano ya mashindano ya vijana, baada ya juzi Zambia kutwaa Kombe la U20.
    Na ukienda kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Equatorial Guinea, hutakuta nchi ya CECAFA zaidi ya nchi za COSAFA, Magharibi na Kaskazini mwa Afrika.
    Hata kwenye mashindano ya vijana ya Afrika, sisi ndiyo tuko nyuma watu wa CECAFA, mfano Tanzania mwaka huu tumetolewa na Afrika Kusini katika U17. Tuna nini sisi. CECAFA yetu, majanga matupu.
    Ndiyo maana mwishoni mwa wiki, COSAFA walikuwa wanafurahia mafanikio yao kufanikisha kumaliza salama mashindano ya U20, huku CECAFA wanajadili matatizo yao ya kushindwa kufanya Challenge, wakati mashindano ya vijana yalikufa zamani na hawana habari nayo. 
    Tena kwenye vikao wanajadili fitina za uchagzui wa FIFA na CAF eti wamuunge mkono nani, badala ya kutafakari kufufua mashindano ya vijana.
    Tuna nini sisi, majanga tu na CECAFA yetu majanga matupu! 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUNA NINI SISI, MAJANGA MATUPU NA CECAFA YETU! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top