• HABARI MPYA

    Friday, February 27, 2015

    NGASSA, MRWANDA NA TAMBWE WAANZISHWA PAMOJA DHIDI YA BDF LEO, SALUM TELELA ‘MASTER’ ATUPWA BENCHI

    Na Mwandishi Wetu, GABORONE
    KOCHA Mholanzi, Hans van der Pluijm amewaanzisha kwa pamoja Mrisho Ngassa, Amissi Tambwe, Simon Msuva na Danny Mrwanda katika safu ya ushambuliaji dhidi ya BDF XI leo. 
    Yanga SC itamenyana na BDF XI leo Saa 1:00 usiku kwa zaa huko na Saa 2:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Awali Kombe la Shirikisho Afrika na Mholanzi huyo amepanga wachezaji wenye kasi watupu mbele.
    Tambwe hana kasi ya kulinganisha na Msuva, Mrwanda na Ngassa, lakini ni mpiganaji pale mbele na ana uwezo mkubwa wa kufunga. 
    Mrisho Ngassa, Simon Msuva na Amissi Tambwe wanaanza pamoja leo dhidi ya BDF
    Huyo ndiye mchezaji aliyefunga mabao yote mawili, Yanga SC ikishinda 2-0 dhidi ya BDF katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam wiki iliyopita.
    Mrwanda ameingia kwenye kikosi cha kwanza kuchukua nafasi ya Mbrazil Andrey Coutinho ambaye ameachwa Dar es Salaam kwa sababu ya majeruhi.
    Safu ya kiungo ya Yanga SC leo itaundwa na Mbuyu Twite chini na juu Haruna Niyonzima- maana yake kiungo ambaye amekuwa akicheza vizuri siku za karibuni, Salum Abdul Telela ‘Master’ anakosekana.
    Hakuna mabadiliko kwenye safu ya ulinzi, Ally Mustafa ‘Barthez’ akianza langoni, kulia Juma Abdul, kushoto Oscar Joshua na katikati Kevin Yondan na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’. 
    Kikosi kamili cha Yanga SC leo; Ally Barthez, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Nadir Cannavaro, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Danny Mrwanda na Mrisho Ngassa.
    Katika benchi watakuwepo Deo Munishi ‘Dida’, Said Juma ‘Kizota’, Hussein Javu, Kpah Sherman, Hassan Dilunga, Salum Telela na Rajab Zahir.
    Azam TV inatarajiwa kuonyeshwa moja kwa moja mchezo huo kutoka Uwanja wa Lobetse kuanzia Saa 2:00 usiku. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGASSA, MRWANDA NA TAMBWE WAANZISHWA PAMOJA DHIDI YA BDF LEO, SALUM TELELA ‘MASTER’ ATUPWA BENCHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top