• HABARI MPYA

    Tuesday, March 03, 2015

    BODI YA LIGI YAMSAFISHA HAJIB, ALIKUWA SAHIHI KUCHEZA DHIDI YA PRISONS, NA ATACHEZA DHIDI YA YANGA SC

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    PRISONS ya Mbeya ilimkatia rufaa mshambuliaji Ibrahim Hajib Migomba aliyeichezea Simba SC katika ushindi wa 5-0 dhidi ya timu hiyo ya jeshi la Magereza mwishoni mwa wiki, ikidai hakustahili kucheza.
    Katika malalamiko yake, Prisons ilidai Migomba alicheza mechi hiyo akiwa ana kadi tatu za njano jambo ambalo walidhani ni kinyume cha kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Hata hivyo, kulingana na mabadiliko ya kanuni za Ligi Kuu, Simba SC ilimtumia Hajib katika mchezo huo baada ya kufuata taratibu na kupewa ridhaa na Bodi ya Ligi.
    Ibrahim Hajib alifunga mabao matatu katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Prisons kabla ya kukatiwa rufaa kwa sababu alikuwa ana kadi tatu za njano

    Kanuni mpya za Ligi Kuu, zinazipa fursa klabu kuchagua mechi za mchezaji kutumikia adhabu za kadi na Simba SC iliiandikia barua Bodi ya Ligi, ikiomba mchezaji huyo acheze mechi na Prisons.
    Pamoja na mechi dhidi ya Prisons, Simba SC ilimuombea pia Hajib acheze dhidi mahasimu, Yanga SC mwishoni mwa wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Hata hivyo, baada ya Hajib kufunga mabao matatu katika ushindi wa 5-0, Prisons wakakata rufaa wakipinga mchezaji huyo kucheza akiwa ana kadi tatu za njano.
    Lakini kumbe SImba SC walikuwa wana barua iliyosainiwa na Mtendaji Mkuu mpya wa Bodi ya Ligi, Fatma Abdallah ikimridhia Hajib kucheza dhidi ya Prisons na Yanga, ili asicheze dhidi ya Mtibwa Sugar katikati ya mwezi huu.
    BIN ZUBEIRY imefanikiwa kuipata nakala ya barua ya Bodi ya Ligi kwenda Simba SC ikimridhia Hajib acheze dhidi ya Prisons na Yanga na akose mechi na Mtibwa.
    Barua hiyo iliyosainiwa na Fatma Abdallah, nakala zake zimetumwa Mwenyekiti wa Bodi, Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kamati ya Waamuzi, Msimamizi wa Kituo cha Dar es Salaam na klabu za Prisons, Yanga SC na Mtibwa Sugar.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BODI YA LIGI YAMSAFISHA HAJIB, ALIKUWA SAHIHI KUCHEZA DHIDI YA PRISONS, NA ATACHEZA DHIDI YA YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top