• HABARI MPYA

    Monday, March 02, 2015

    MACHACHE NINAYOFAHAMU KUHUSU KAPTENI JOHN KOMBA

    WABUNGE wengi wamekuwa wakishinda kwenye chaguzi kwa msaada mkubwa wa sauti ya Kapteni John Damian Komba, marais wengi wa hapa nchini hadi wa baadhi ya nchi za jirani nao pia hawakukwepa mchango wa sauti ya Komba kushinda nyadhifa hizo. Hakika Komba alikuwa ni msanii wa kipekee ambaye ananilazimisha kuzitumia Aya zangu 15 za kila Jumatatu kuandika machache ninayoyafahamu juu yake. 
    Alipotunga wimbo wa maombolezo ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere mwaka 1999, taifa likazidi kuzizima kwa sauti yake nzito iliyofanya mambo mawili ambayo ni nadra sana kwenda sambamba – kuhuzunisha na kufariji.

    Ilikuwa ni kazi iliyotoka kwa haraka sana mara tu baada ya kifo cha Nyerere kutangazwa …unaweza ukadhani kuwa labda kwa vile Mwalimu aligua kwa muda mrefu basi pengine hali hiyo iliweza kumpa Komba muda wa kujiandaa kuutunga. Utakuwa unakosea sana. Mwaka 1986 mwezi Oktoba, Komba alitunga wimbo wa kifo cha Samora Machel muda mfupi tu baada ya rais huyo wa Msumbiji kufariki dunia kwa ajali ya ndege kwenye ardhi ya Afrika Kusini.
    Komba - mbunge wa Mbinga Magharibi na Mkurugenzi wa kundi la sanaa za maonesho la Tanzania One Theatre (TOT) - ambaye alifariki dunia Jumamosi mchana, alijaaliwa sauti yenye hamasa ambayo inapoanza tu kusikika ni lazima utaisikiliza na kuruhusu ujumbe kupenya kwenye masikio yako bila kujali kuwa unampenda au humpendi, anakuudhi au kukufurahisha.
    Marehemu Kapten Komba alianza kujiingiza katika masuala ya muziki tangu akiwa shule ya msingi nyumbani kwao Litui, Mbinga, kandokando mwa ziwa Nyasa kwa kufundishwa kuimba na mapadri wa kizungu.
    Alipoingia sekondari akapewa jukumu la kuwa kiranja wa starehe na utamaduni kutokana na kuonyesha kipaji na uwezo mkubwa kwenye fani mbalimbali za burudani, kama vile kwaya, jiving na ngoma za kienyeji.
    Alipohitimu masomo yake ya sekondari, mwaka 1975, alijiunga na chuo cha ualimu Kleruu, Iringa alikotwaa cheti cha Daraja ‘A’ cha taaluma hiyo, kabla ya mwaka 1976 kujiunga na JKT na kwenda Mafinga, Iringa kwa mujibu wa sheria.
    Akiwa Mafinga Komba akakutana na Brigedia Jenerali Mosses Nnauye aliyekihusudu kipaji chake na kuamua kukiendeleza kwa kumwimbisha zaidi kwenye magwaride na nyimbo nyingine mbalimbali za kijeshi. Komba akawa akitunga nyimbo na kuimba, huku Nnauye akipiga kinanda.
    Komba aliingia vipi jeshini? Mwaka 1977 alikwenda kufundisha shule ya msingi Gangilonga, mkoani Iringa lakini mwaka uliofuata, 1978 Nnauye akamfuata na kumpeleka Mondoli, katika chuo cha jeshi na kuhitimu mafunzo na kutunukiwa nyota moja na alipotoka hapo akapokewa moja kwa moja na vita ya Kagera.
    Mwaka 1980 akachaguliwa kuwa kiongozi wa kikundi cha jeshi cha sanaa za maonyesho, ambako alisafiri nacho katika nchi za Zimbabwe, Msumbiji, Kenya, Zambia, Libya, Seychelles na Urusi na akaanza kujipenyeza kwenye siasa mwaka 1987 pale alipoamua kugombea nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) ambayo alishinda na kudumu nayo hadi mwisho wa uhai wake.
    Mwaka 1988 neema ikazidi kumdokea Kapteni Komba ambapo CCM ilimpeleka barani Ulaya kusomea elimu ya siasa kwa miaka miwili, na kuibuka na stashahada. Mwaka 1992 akaamua kufanya maamuzi magamu, akaacha kazi ya jeshi na kuamua kuitumikia CCM na moja kwa moja akateuliwa kuwa mkurugenzi wa kundi jipya la Tanzania One Theatre (TOT) lililoanzishwa mahsusi na chama hicho tawala kwaajili ya propaganda za kukabiliana na changamoto za ujio wa siasa za vyama vingi.
    Kazi ya kwanza kabisa ya Komba katika TOT ikazaa wimbo “CCM Nambari Wani” ambao hadi leo hii bado ni nguzo kubwa ya Chama Cha Mapinduzi katika mikutano ya kampeni za kisiasa na hadi ndani ya vikao muhimu vya chama hicho.
    Mwaka 2005 Komba aliyeacha mke na watato 10, akagombea ubunge jimbo la Mbinga Magharibi kwa tiketi ya CCM na kushinda, nafasi ambayo pia ameitumikia hadi kifo chake.
    Komba hakuwa mtu wa makuu, alicheka na kutaniana na kila mtu, binafsi nimebahatika kuwa karibu na Kapteni Komba, alikuwa akiniamini kwenye kazi zake na hakuthubutu kumwamini mshindani wangu yeyote yule, nilimkera mara kadhaa lakini bado hakunikimbia, alichokuwa akikifanya ni ‘kunichana’ bila kupepesa macho baada ya hapo kisirani kinamwisha na maisha yanaendelea. Nashukuru kuwa fulana za msiba wake nimezichapicha kwa mkono wangu mwenyewe, nina uhakika kama jambo hilo angeulizwa ukingoni mwa uhai wake basi jibu lake lingekuwa moja – Said Mdoe. 
    Huyo ndiye Kapteni Mstaafu, John Damian Komba aliyezaliwa mwaka 1954, Lituhi, Mbinga mkoani Ruvuma na kupata elimu katika shule ya msingi Lituhi, Mbinga, Ruvuma kati ya mwaka 1962 na mwaka 1968 kabla ya kujiunga na sekondari ya Songea Boys kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1974.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MACHACHE NINAYOFAHAMU KUHUSU KAPTENI JOHN KOMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top