• HABARI MPYA

    Tuesday, March 31, 2015

    MKASA WA KUSIKITISHA WA ULIMWENGU TP MAZEMBE…ALIPELEKA OFA YA KWENDA ULAYA MKONO KWA MKONO, LAKINI AKACHOMOLEWA

    Na Mahmoud Zubeiry, MWANZA
    MSHAMBULIAJI wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu amesema kwamba hafurahii maisha katika klabu yake hiyo na sasa anataka kuondoka, lakini kila ofa inayokuja ‘inatiwa kapuni’.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY juzi mjini hapa, Ulimwengu, mshambuliaji mwenye nguvu, kasi na uwezo mkubwa wa kuwapita mabeki, alisema kwamba mmiliki wa klabu yao, Moise Katumbi Chapwe amekuwa akiwabania kuondoka.
    “Inaniuma sana hadi sasa bado nacheza Afrika, zinakuja ofa nyingi tunatakiwa na klabu za Ulaya, lakini bosi anakataa, kisa bado tuna Mkataba na timu,”amesema Uli.
    Mshambuliaji huyo wa zamani wa Moro United, amesema kwamba anapojaribu kwenda kumuulizia bosi wake huyo juu ya ofa hiyo amekuwa kama ‘akipotezea’.
    Thomas Ulimwengu alipeleka ofa ya klabu ya Ulaya, TP Mazembe wakamkatalia kuondoka 

    “Kuna wakati baada ya kusemea hajapata ofa ya klabu moja ambayo nilikuwa nina uhakika imefika, ikabidi niwaambie wale jamaa wanitumie mimi nimpelekee yeye mkono kwa mkono, lakini pamoja na kufanya hivyo, bado alizungua,”amesema Ulimwengu.
    Mshambuliaji huyo tegemeo wa Tanzania kwa sasa amesema kwamba kwa sasa anasubiri tu kumaliza Mkataba wake mwakani, ili aangalie ustaarabu mwingine.
    Lakini Ulimwengu amesema inamuuma sana katika wakati huu ambao klabu nyingi za Ulaya zinamtaka, Mazembe inambania.
    “Yaani imefika wakati sikufichi ndugu yangu, nafurahi tu kwa sababu pale nakubalika, nina marafiki, mashabiki wananikubali, lakini nikifikiria kwamba napoteza nafasi za kusogea mbele, nakosa furaha kabisa,”amesema.
    Pamoja na hayo, Ulimwengu amesema hakati tamaa, ataendelea kuitumikia Mazembe kwa uadilifu wa hali ya juu hadi hapo atakapomaliza Mkataba wake aondoke salama.       
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKASA WA KUSIKITISHA WA ULIMWENGU TP MAZEMBE…ALIPELEKA OFA YA KWENDA ULAYA MKONO KWA MKONO, LAKINI AKACHOMOLEWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top