• HABARI MPYA

    Wednesday, April 01, 2015

    BARCELONA KUTUA ZANZIBAR APRILI 9

    Na Salum Vuai, ZANZIBAR
    KIKOSI cha wachezaji wa zamani wa klabu ya FC Barcelona ya Hispania, kinatarajiwa kuwasili Zanzibar Aprli 9, mwaka huu kwa ziara ya siku moja.
    Msafara huo utakaokuwa na watu 32 wakiwemo wachezaji 28 na viongozi wanne, utaongozwa na mwanandinga wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, Johan Cruyff, aliyewika katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1974 yaliyofanyika nchi iliyokuwa Ujerumani Magharibi, na 1978 nchini Argentina.
    Akizungumza na waandishi wa habari leo, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Saleh Ramadhan Feruzi alisema, ziara hiyo inakuja baada ya magwiji hao kukubali mwaliko wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
    Mmoja wa magwiji wa Barcelona wanaotarajiwa kuzuru nchini, Patrick Kluivert

    Feruzi alisema ujio huo ni sehemu ya ziara ya siku nne ya maveterani hao nchini Tanzania itakayoanza Aprili 7 jijini Dar es Salaam.
    Alieleza kuwa malengo makuu ya ziara hiyo kwa Zanzibar, ni kupata fursa ya kuvitangaza visiwa hivyo pamoja na vivutio vyake vya utalii, ili kuvutia wageni wengi zaidi kila mwaka.
    Lengo jengine, alisema ni kuwapa fursa magwiji hao wa soka kushuhudia vipaji vya wachezaji wadogo wa ngazi za ‘Juvenile, Junior na Central’, pamoja na kutoa maelekezo juu ya mbinu mbalimbali za kusakata kabumbu.
    Akizungumzia ratiba ya ziara hiyo, Feruzi alisema baada ya msafara huo kuwasili asubuhi ya Aprili 9 katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume, wanasoka hao watatembelea mashamba ya viungo, Mji Mkongwe ambako wataangalia majengo ya kihistoria kama Beit El Ajaib, Makumbusho ya Kasri, Ngome Kongwe, sambamba na mtaa wa Gizenga na maeneo yanayokaribiana nao.
    Hali kadhalika, katika bustani ya Forodhani, watapigiwa taarab asilia kwa dakika chache ili kupata ladha halisi ya visiwa vya Zanzibar vyenye mchanganyiko wa tamaduni za asili mbalimbali.
    Aidha baada ya hapo, Feruzi alisema wachezaji hao maveterani watakwenda kuonana na Rais Dk. Shein Ikulu mjini Zanzibar.
    Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kuanzia saa 11:00 hadi 12:30 jioni, watakuwepo uwanja wa Amaan ambako watashuhudia wachezaji wadogo wakionesha ufundi wa kucheza na mpira.
    Vijana hao pia wataunda timu mbili zitakazopambana, ili kuwapa fursa wakongwe hao kujionea vipaji vya soka vilivyosheheni hapa Zanzibar, kabla kikosi cha wachezaji 11 cha chipukizi hao kuwavaa wanasoka wa Barcelona Veterans, mchezo utakaochukua dakika 45.
    “Katika mechi hii, magwiji wa Barca watakuwa wakiwafundisha wachezaji hao wa Zanzibar mbinu nzuri za kucheza. Kwa mfano, wakipata ‘free kick’ na kupiga, wataoneshwa vipi wapige na kufanya hivyo,” alifafanua Feruzi.
    Mbali na kuwataka Wazanzibari waoneshe ukarimu na kuwapokea vizuri wanandinga hao wa zamani kila watakapopita, Feruzi pia aliwaomba wahudhurie kwa wingi uwanja wa Amaan ambako pia makocha wa madaraja tofauti wa Zanzibar watakuwepo kunufaika na ziara ya wanasoka hao.   
    Mbali na Cruyff, baadhi ya wachezaji wengine waliothibitisha kuwemo kwenye ziara hiyo, ni Patrick Kluivert, Edgar Jones, Eric Abidal na Decco.
    Aidha yumo mtoto wa mchezaji bora wa zamani wa Ureno aliyekuwa raia wa Msumbiji kabla hajabadili uraia, Eusebio da Silva Ferreira, Eusebio Jr. ambaye ameitwa kwa heshima ya baba yake aliyefariki dunia Januari 5, 2014 akiwa na umri wa miaka 71.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BARCELONA KUTUA ZANZIBAR APRILI 9 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top