• HABARI MPYA

    Tuesday, April 21, 2015

    YANGA SC NCHI YOTE YAO, WAIBAMIZA STAND UNITED 3-2 TAIFA, BADO POINTI SITA UBINGWA

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imeendelea kuitumulia vumbi Azam FC katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia ushindi wa mabao 3-2 jioni ya leo dhidi ya Stand United Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga SC sasa wanafikisha pointi 49 baada ya kucheza mechi 22- maana yake wanahitaji pointi sita zaidi kujihakikishia ubingwa unaoshikiliwa na Azam FC kwa sasa.
    Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm leo alimuanzisha kwa mara ya kwanza kipa Deo Munishi ‘Dida’ tangu Desemba 12 mwaka jana alipotunguliwa mabao mawili Yanga ikilala 2-0 mbele ya watani, Simba SC katika mechi ya Nani Mtani Jembe.
    Wafungaji wa mabao ya Yanga SC leo, Mrisho Ngassa kulia, Simon Msuva (katikati) na Amisi Tambwe kushoto

    Lakini Yanga SC iliendelea kukosa huduma ya kiungo wake hodari, Salum Abdul Telela ‘Master’ anayesumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu. 
    Hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao 2-1 yaliyofungwa na Amisi Tambwe na Mrisho Ngassa, japokuwa Stand United ndiyo waliotangulia kufunga kupitia kwa Kheri Khalifa. 
    Yanga SC iliuanza mchezo kwa kasi na dakika ya nne, Mbrazil Andrey Coutinho aliyekuwa anacheza kwa mara ya kwanza tangu Februari 22 alipoumia goti katika mchezo dhidi ya Mbeya City, alifumua shuti kali baada ya pasi ya Haruna Niyonzima akiwa ndani ya boksi, lakini likatoka nje kidogo.
    Dakika ya 12, mshambuliaji hatari wa Stand, Mnigeria Abasalim Chidiebele alifunga bao akimalizia pasi ya Pastory Athanas, lakini refa Ahmada Simba akalikataa akidai kabla ya kufunga kuna madhambi yalitendeka.
    Dakika ya 17 Coutinho tena alikaribia kuifungia Yanga SC bao, baada ya krosi ya winga Simon Msuva iliyoguswa kidogo na Tambwe kwa kichwa, lakini shuti lake likaokolewa na kipa Hamad Juma wa Stand na kuwa kona ambayo haikuwa na madhara.
    Dakika ya 21 Stand wakapata bao safi kupitia kwa Kheri Khalifa, aliyemalizia mpira wa adhabu wa Haroun Chanongo na kuwaacha mabeki wa Yanga SC wakiwa wamezubaa wakidhani ameotea.
    Tambwe aliunganisha kwa kichwa kona ya Msuva dakika ya 28, lakini mpira ukapaa juu kidogo na kuwaacha mashabiki wa Yanga SC ‘wakitapika’ jukwaani.
    Hatimaye mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodcom Tanzania Bara msimu uliopita, Tambwe akakata kiu yake dakika ya 30 baada ya kuisawazishia Yanga SC, akimalizia kazi nzuri ya Ngassa aliyewatoka mabeki na kupiga krosi maridadi.
    Ngassa mwenyewe, ambaye jana amemaliza Mkataba wake Yanga SC aliifungia timu hiyo bao la pili dakika ya 45 akimalizia pasi ya beki wa kulia, Juma Abdul.
    Kipindi cha pili, Yanga SC walirudi na kasi na dakika ya 52 almanusra Coutinho afunge kwa mpira wa adhabu kama shuti lake lisingegonga mwamba wa juu na kutoka nje, kufuatia Ngassa kuangushwa nje kidogo ya boksi.
    Mrisho Ngassa akimtoka beki wa Stand United
    Andrey Coutinho akitafuta maarifa ya kumtoka beki wa Stand United
    Amisi Tambwe akimtoka beki wa Stand Uited

    Stand ilijibu shambulizi hilo dakika nne baadaye, baada ya Dida kuudaka mpira wa kichwa uliopigwa na Chidiebele akiwa ndani ya boksi, kufuatia krosi ya Chanongo.
    Stand United walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 67 kupitia kwa Kheri Khalifa, aliyepokea pasi ya Chidiebele na kuwazidi maarifa mabeki wa Yanga SC.
    Yanga SC ilipata bao la ushindi dakika ya 79 kwa mkwaju wa penalti wa Simon Msuva ambaye hilo linakuwa bao lake la 13 msimu huu katika Ligi Kuu, kufuatia mshambuliaji Amissi Tambwe kuangushwa kwenye boksi na beki wa Stand United, Peter Mutabuzi. 
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Mbuyu Twite, Said Juma, Simon Msuva/Hussein Javu dk80, Haruna Niyonzima, Amsi Tambwe, Mrisho Ngassa/Danny Mrwanda dk90 na Andrey Coutinho/Kpah Sherman dk58.
    Stand United: Hamadi Juma, Revocatus Mgunga, Abuu Ubwa, Jisend Mathias, Peter Mutabuzi, John Janga, Hamisi Shengo, Pastory Athanas/Reyna Mgungira dk89, Kheri Khalifa/Chinedu Nwankwoze dk76, Abasalim Chidiebele/Vitalis Mayanga dk89 na Haroun Chanongo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC NCHI YOTE YAO, WAIBAMIZA STAND UNITED 3-2 TAIFA, BADO POINTI SITA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top