• HABARI MPYA

    Friday, May 22, 2015

    KOCHA WA IVORY COAST ABWAGA MANYANGA, ATIMKIA UFARANSA

    KOCHA Mfaransa, Herve Renard ameachia ngazi timu ya taifa ya Ivory Coast.
    Mshindi huyo wa Makombe mawili ya Mataifa ya Afrika anaamua kuondoka baada ya kuipa timu hiyo taji la AFCON katika mashindano yaliyofanyika Equatorial Guinea Februari mwaka huu.
    Na hatua hiyo inafuatia kupata kazi ya kwenda kuifundisha klabu ya Ligue 1 Ufaransa, LOSC Lille kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari nchini humo.
    Lille imeachana na kocha Rene Girard, ambaye anaweza kulipwa Euro 800 000 kuvunja Mkataba. Mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 46 anatarajiwa kusaini Mkataba wa miaka mitatu na Lille.
    Kocha Herve Renard aliyeipa pia Zambia ubngwa wa AFCON anarejea kwao Ufaransa kuifundisha klabu ya Lille

    Renard, ambaye aliifundisha pia Sochaux misimu miwili iliyopita kabla ya kutua Ivory Coast, anatarajiwa kuungana na rafiki yake, Patrice Beaumelle kama Msaidizi wake.
    Imethigitishwa kwamba Ivory Coast sasa itatafuta mbadala wake haraka kabla ya kuanza kwa mechi za kufuzu AFCON mwaka 2017 Tembo hao wakianza na Gabon Juni 13.
    Kocha Herve Renard anaondoka huku soka ya Ivory Coast ikiwa katika mgogoro mzito kufuatia kashfa ya kuibwa kwa dola za Kimarekani 800,000 za posho za wachezaji na makocha baada ya ushindi wa Kombe la AFCON mapema mwaka huu.
    Kashfa hiyo imefanya Waziri wa Michezo wa Ivory Coast, Alain Lobognon afukuzwe kazi baada ya Rais wa nchi hiyo, Alassane Ouattara kuagiza uchunguzi ufanyike juu ya wizi huo wa dola hizo za Kimarekani 800 000.
    Meneja Uhasibu wa taifa alifukuzwa wiki iliyopita, muda baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani kuanzisha uchunguzi wa kashfa hiyo.
    Wizira ya Michezo na Shirikisho la Soka wamekuwa wakinyoosheana vidole tangu mwezi uliopita baada ya wachezaji kuvujisha siri kwamba hawakulipwa posho zao.
    Baada ya kurejea kutoka AFCON, kila mchezaji aliahidiwa kupewa dola 97, 000 (dola 50, 000 wakipewa nyumba na dola 47, 000 fedha taslimu.
    Kocha Herve Renard alitakiwa kupewa dola 123, 000 wakati dola 490, 000 wangegawana wasaidizi wake katika benchi la Ufundi.
    Pamoja na hayo, kiungo wa VfB Stuttgart, Serey Die akasema mapema Aprili kwamba walipewa sehemu kidogo tu ya fedha hizo, wakati kocha huyo Mfaransa, Renard akathibitisha hajapata haki yake.
    Rais ameamua kuvalia njuga suala hilo baada ya kuona Wizara ya Michezo na FA wameshindwa kulipatia ufumbuzi. Tembo waliwafunga Ghana katika fainali kutwaa taji hilo la pili katika historia yao kwenye michuano hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA WA IVORY COAST ABWAGA MANYANGA, ATIMKIA UFARANSA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top