• HABARI MPYA

    Saturday, May 23, 2015

    NOOIJ AWAKWAMA TFF, HAKUFUZIKI…TUNAYE TU HADI TUKOME WENYEWE!

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    TIMU ya soka ya taifa yaTanzania, Taifa Stars inarejea leo baada ya kuboronga kwenye michuano ya Kombe la COSAFA ikirejea bila ushidi, kufuatia kufungwa mechi zote, lakini kocha Mart Nooij hatafukuzwa.
    Mholanzi huyo ataendelea na kazi kwa hoja moja tu ya msingi, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halina fedha za kumlipa kuvunja naye Mkataba, ambao unamalizika Mei mwakani. 
    Kamati ya Utendaji ya TFF itakutana kesho Dar es Salaam kujadili mwenendo wa timu zote za taifa na ajenda kubwa inatarajiwa kuwa Nooij, ambaye katika mechi 16 alizoiongoza Stars tangu awasili mwishoni mwa Aprili kuchukua mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen ameshinda tatu tu, akifungwa sita na sare sita.
    Hafukuziki; Kocha Mart Nooij ataendelea kufanya kazi Tanzania hadi Mei mwakani

    Stars imefungwa mechi zote tatu za COSAFA 1-0 na Lesotho jana 2-0 na Madagascar Jumatano na 1-0 na Swaziland Jumatatu.
    TFF ilihadaika na wasifu mzuri wa Nooij aliyetua Tanzania akitokea klabu ya St George ya Ethiopia Aprili mwaka jana na kumpa Mkataba mnono. 
    Wasifu wa Nooij unasema amewahi kuwa mwalimu maalum katika programu za maendeleo ya soka katika Chama cha Soka Uholanzi (DFA) na pia amewahi kufundisha timu ya EVC 1913 ya Marekani na baadaye Kazakhstan.
    Alikuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Burkina Faso katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2003 na mwaka 2004 alikuwa kocha wa muda wa klabu ya FC Volendam ya Uholanzi.
    Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa kocha wa Msumbiji na akaiwezesha kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza Mambas wanashiriki AFCON baada ya msoto wa miaka 12. 
    Hata hivyo, katika fainali hizo, Msumbiji ilishika mkia katika kundi lake baada ya kuambulia sare moja na kufungwa mechi mbili. Baada ya kukosa tiketi ya AFCON 2012, Nooij akajiuzulu Septemba mwaka 2011 na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani, Gert Engels.
    Aprili 19 mwaka 2012, aliajiriwa na klabu ya Santos ya Afrika Kusini, ambako hata hivyo alifukuzwa Desemba 18, mwaka 2012 na kuhamia St George ya Ethiopia kabla ya kuja Tanzania Aprili mwaka jana. 
    Nooij sasa ataiongoza Stars katika mechi za kufuzu AFCON ikianza na Msiri Juni 13 wakati Julai itakuwa mchezo wa kufuzu CHAN dhidi ya Uganda.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NOOIJ AWAKWAMA TFF, HAKUFUZIKI…TUNAYE TU HADI TUKOME WENYEWE! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top